Rais
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote wa
Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge
wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya
ya Bariadi Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao
walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe
Taarifa
iliyotolewa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo
ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana
matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika
shughuli za maendeleo ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
Viongozi
waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na
Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri
za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao
huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi
hufikia takribani 1,500.
Kwa
kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na
Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka
17 iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya
kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya
kuienzi siku hiyo.
Aidha,
Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika
shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao,
zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za
Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa
utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa
Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na
Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi
na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya
tarehe 14 Oktoba, 2016.
Mgeni
Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed
Shein.
No comments:
Post a Comment