TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO)
Mhandisi Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji mkubwa
wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya
ujenzi wa reli ya kati.
Akitoa taarifa kwa
vyombo vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais
Magufuli amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka
Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji
wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard
Gauge"
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
Amesema pamoja na kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO baada ya
kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato
wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika
Aidha Rais
Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa
ushirikiano kwa vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu
mchakato wa Zabuni hiyo.
Pia ameiagiza
Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua
dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo
itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua
nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli
Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia
ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.

No comments:
Post a Comment