WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefurahishwa na hali ya chakula mkoani Ruvuma,
ikiwa kati ya mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi
nchini.
Akizungumza
na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali jana katika
ukumbi uliopo Ikulu ndogo Songea, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa
mkoa kuhakikisha kuna upatikanaji wa masoko kwa mazao mbalimbali
pamoja na kuendelea kutoa msukumo kwa wananchi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa
Pia,
amewapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kutoa msukumo kwa wananchi na
kufanyakazi, na kusema ni jambo linalosaidia kupanda kwa pato la mtu
mmoja mmoja, hata hivyo hakusita kuwashukuru kwa mapokezi makubwa
aliyopata.
“Nawapongeza
sana wana Ruvuma kwa kuongeza pato la ndani kutoka kutoka shilingi
654,227, hadi kufikia shilingi 1,800,000 kwa kipindi cha mika 4
tuendelee kujiweka vizuri kwa kuongeza pato la mtu mmoja mmoja”
alisema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu Majaliwa pia amesisitiza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo
yote yenye mabonde ili wakulima waweze kuvuna bila kutegemea sana
kipindi cha masika. Amesema ni lazima kuimarisha huduma muhimu na
kusisitiza matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana katika mazao
hayo.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu amesema
zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Ruvuma hutegemea kilimo cha mazao
mbalimbali ya chakula na biashara yakiwemo mahindi, mpunga ambao
unalimwa sehemu za Tunduru na Songea vijijini, korosho ambazo
zinalimwa sehemu za Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea
vijijini na tumbaku maeneo ya Namtumbo,Mbinga na Songea vijijini.
Alisema,
Ruvuma imekua ikizalisha chakula kwa kiwango cha utoshelezi na ziada
kwa kipindi cha mwaka 2012 - 2013, 2013 - 2014 hali hiyo imeendelea
kuwa nzuri hadi kipindi cha mwaka 2015 - 2016. Mahitaji yakiwa ni
tani 469,172 na ziada ikiwa tani 1,950,111, ametaja baadhi ya sababu
za ongezeko hilo la tani ni pamoja na matumizi ya dhana bora za
kilimo, matumizi ya pembejeo za kisasa na urahisi wa upatikanaji wa
pembejeo, aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Waziri
Mkuu Majaliwa ambaye jana (Jumapili, Januari 3, 2016) ameanza ziara
ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma, kesho siku ya jumatatu atakuwa
na shughuli za kufungua tawi la Benki ya Posta mjini Songea, kukagua
maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) kanda ya
Songea na kukagua Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Kupitia
ziara hii Serikali ina lengo la kuona hali halisi ya utendaji wa
shughuli za maendeleo kutoka kwa watendaji mbalimbali, kuwatia moyo
na kuweka msisitizo katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika
sekta ya Afya.

No comments:
Post a Comment