Kiwango cha umri wa kuishi kwa
Watanzania kimeongezeka kutoka miaka 51 hadi miaka 61 katika kipindi
cha miaka kumi iliyopita sababu kuu ikiwa ni maboresho yaliyofanyika
katika sekta ya afya nchini.
Naibu waziri wa afya Dkt Khamis
Kigwangala, amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti
wa kutathmini utoaji wa huduma za afya nchini, utafiti uliofanywa na
ofisi ya taifa ya takwimu-NBS.
Naibu waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Dkt Khamis Kigwangala
Kwa mujibu wa Dkt Kigwangala,
mafanikio hayo katika sekta ya afya yameiwezesha nchi kuvuka kutoka
katika kundi la nchi maskini na kuingia kwenye kundi la nchi za
uchumi wa kati kwa upande wa sekta ya afya.
Naibu waziri Kigwangala ametaja
maeneo yaliyofanikiwa kuwa ni katika upatikanaji wa huduma za uhakika
za maji na nishati katika vituo vya tiba, huku maeneo mengi ya utoaji
huduma za afya nchini yakiwa na wataalam wenye ujuzi unaohitajika
katika maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu
ofisi ya Taifa ya Takwimu Dr Albina Chuwa amesema kuwa bado kuna
changamoto ya wahudumu wa afya kupatiwa mafunzo ya ziada ili kuweza
kukabiliana na vipimo mbalimbali na sera za afya zifanye kazi
iliyotakiwa kwakutumia Takwimu mbalimbali nchini.

No comments:
Post a Comment