Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema
mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza
fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni.
Agizo
hilo la Rais Dk. Magufuli limetolewa leo na Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika
ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Mhe.
Majaliwa amesema wakati akifungua mafunzo ya Mawaziri na Naibu Waziri
kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa
Ahadi ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu jana alikabidhiwa majina ya
Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao hawajawasilisha Tamko la Rasilimali
na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.
Amewataja
mawaziri wanaotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na
hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Bw. Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira), Bw. January Makamba.
Wengine
ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga ambaye
anatakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce
Ndalichako ambaye anatakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mazingira), Bw. Luhaga Mpina anatakiwa kurejesha fomu za tamko la
rasilmali na madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi
wa umma.

No comments:
Post a Comment