Waziri wa nchi ofisi ya rais tawala
za mikoa na serikali za mitaa Tamisemi George Simbachawene ameuagiza
uongozi wa mkoa wa Iringa kuwatafutia maeneo ya makazi ya kudumu
waathirika wa mafuriko.
Waathirika hao wanaendelea kuokolewa
kwenye mafuriko katika mashamba ya mpunga Pawaga ili kuhakikisha
hakuna mtu anayerudi kuweka makazi ya kudumu katika maeneo hayo ili
eneo hilo libakie la mashamba pekee.
Waziri Simbachawene amesema hayo
alipowatembelea waathirika wa mafuriko waliookolewa kutoka kwenye
mashamba ya mpunga Pawaga walikokuwa wamezungukwa na maji na kusema
kuwa kuanzia sasa serikali inapiga marufuku vibanda vya muda pamoja
na nyumba za kudumu kwenye mashamba hayo ili kuepusha kujirudia kwa
janga hilo.
Waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Tamisemi George Simbachawene
Akitoa taarifa ya zoezi la uokoaji
kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Iringa Bibi Lucy Nyalu amesema
mpaka sasa watu walio kwenye kambi za muda wamefikia 419 ambapo idadi
hiyo imepungua kutokana na baadhi yao kuchukuliwa na ndugu zao ama
kuondoka makwao.
Waziri Simbachawene ameupongeza
uongozi wa mkoa wa Iringa kwa juhudi za uokoaji zinazoendelea hadi
sasa kukiwa hakuna kifo hata kimoja kilichokwisharipotiwa licha ya
changamoto za ukosefu wa vifaa vya uokoaji na kuwaomba wadau
mbalimbali kushirikiana na serikali kusaidia waathirika hao kwa hali
na mali ambapo mkuu wa mkoa wa Iringa Bibi Amina Masenza amewataka
waathirika hao kudumisha usafi ili kujiepusha na maambukizi ya
ugonjwa wa kipindupindu.
Mapema kabla ya ziara ya waziri
George Simbachawene shirika la afya duniani WHO limekabidhi vifaa
mbalimbali ikiwemo dawa za kusafisha maji zenye thamani ya shilingi
milioni 25 kwa lengo la kusaidia kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa
kipindupindu kwenye kambi hizo za waathirika wa mafuriko huku waziri
Simbachawene akikabidhi shilingi mil.5 zilizochangwa na watumishi wa
ofisi yake..
No comments:
Post a Comment